Fanya Hivi Uone Nguvu ya Ajabu Katika Kushukuru.

Ipo nguvu ya ajabu isiyoweza hata kuelezeka pindi mmoja anapozama katika kushukuru kwa moyo mkunjufu.

Shukrani yoyote ya kweli huzaa matunda mazuri yasiyotarajiwa.Tuanze kuangalia biblia inasemaje kuhusu hili;
 
” Wanafunzi wake wakamwambia, Tupate wapi mikate mingi hapa nyikani, hata kushibisha mkutano mkuu namna hii? Yesu akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba, na visamaki vichache. 
Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akashukuru akavimega, akawapa wanafunzi wake, nao wanafunzi wakawapa makutano. ” Mathayo 15:33-36
Katika andiko hili,Bwana Yesu anatufundisha leo kwamba ipo nguvu kubwa ipatikanayo katika kushukuru.Biblia inatueleza idadi ya mikate kwamba ilikuwa ni mikate saba,na visamaki vichache ambayo ndio ilikusudiwa na wanafunzi wake kuulisha mkutano mkuu namna ile.
Wanafunzi wa Bwana,hawakuijua siri iliyopo katika kushukuru,kwamba kuna nguvu kubwa katika kushukuru. Neno la Mungu halituambii kwamba Bwana Yesu alimkemea shetani kwa sababu ya uchache wa mikate na visamaki,wala neno la Mungu halisemi ya kwamba Yesu alingangana kuomba mikate mingine ishuke kutoka mbinguni ili makutano washibe,bali neno linasema alishukuru,kisha akamega…
Sipati picha kama tungelikuwa sisi walokole wa leo katika mazingira kama hayo tungelifanyeje,Je tungekaza kushukuru kama alivyofanya Bwana Yesu,au tungevunja na kubomoa hila za shetani ? Sijui,jibu unalo wewe unafikiri mlokole wa leo ang’eombaje?
Nimekuuliza hivyo kwa sababu leo wapo wapendwa,wao wanajua maombi ya aina moja tu,maombi ya kuvunja na kubomoa na kuteketeza hila za shetani basi !,huku wakiwa wamesahau kuwa kushukuru pia ni aina ya maombi yenye nguvu.
Sikia;
Mikate ile mitano na visamaki vichache walivyokuwa navyo wanafunzi wa Yesu,ndivyo hivyo hivyo ambavyo Yesu alivitwaa kutoka kwao. Alipovitwaa, havikubadilika vilikuwa vile vile. Lakini kilichobadilisha ni maombi ya kushukuru aliyeyofanya Bwana Yesu,kisha muujiza ukatokea wa kuongezeka kwa mikate na samaki hatimaye kuulisha mkutano mkuu.
~ Kumbe kushukuru ni aina ya maombi,ahaa nimegundua basi leo.Ok,basi nini maana ya kushukuru?
▪ Kushukuru ni tendo la imani linaloelezea furaha ya moyo wa mtu katika yale aliyoyaona na kuyapata katika macho ya damu na nyama au katika macho ya rohoni.
Nisemambo kwamba  ” tendo la imani ” hii ina maana kushukuru ni moja ya aina ya maombi. Na maombi yoyote husimama katika imani,na ndio maana yeye aombaye huomba kisha uamini kwamba yale aliyoyaomba yamekuwa yake,hata kama hajayashika na kuyaona dhahili, lakini ndivyo aaminivyo. ( Marko 11:23 )
Chukua tafsiri hiyo ya kushukuru,kisha tuangalie tena Mathayo 15:33-36 ( Andiko lililopo hapo juu ). Utagundua kwamba;
▪ Bwana Yesu,alifanya tendo la imani ( aliposhukuru ).
~ Kwa maana shukrani ni tendo la imani lifanyikalo penye madhabahu ya Bwana Mungu aliye hai. Mikate na visamaki vilibidi vipelekwe katika madhabahu ya Bwana ambaye Yesu mwenyewe ndio madhabahu ya Bwana. 
Jambo hili pia tunaliona likifanywa mara nyingi na watu wa Mungu katika biblia. Mfano Ibrahimu,mara nyingi ambapo Bwana akimtokea basi mahali hapo ni lazima atengeneze madhabahu kisha na kutoa sadaka ya shukrani kwamba Bwana amemtokea hapo.
Tazama hata kwa Nuhu, Biblia inasema;
” Nuhu akamjengea Bwana madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. ” Mwanzo :8:20
Baada ya Nuhu kuponwa na gharika,ndiposa akamjengea Bwana madhabahu kisha akamshukuru Bwana Mungu kwa sadaka nzuri. 
Sadaka hii ilikuwa ni sadaka ya shukrani ambayo imetolewa katika madhabahu,na biblia inasema kwamba Mungu aliposikia harufu nzuri ya kumridhisha Bwana akasema hatailaani tena nchi. Nuhu alijua siri ya kushukuru.
▪ Bwana Yesu,aliweza kueleza furaha ya moyo wake,katika vile visamaki na mikate aliyoitwaa,na kuona ongezeko la ajabu ndani yake kabla hajawapea wanafunzi wake ili wanafunzi nao wawapee makutano.
Watu wengi hushindwa kumshukuru Mungu kwa vile walivyovipata. Kwa kisingizio eti ni vidogo mno,wakisubiri wapate vikubwa eti ndipo wamshukuru Mungu. 
Lakini sivyo tunavyofundishwa leo na Bwana Yesu,maana Yeye alipovitwaa visamaki na mikate saba, alimshukuru Mungu kwa vile vile vijisamaki vichache.
Hivi unafikiri laiti kama Bwana Yesu angelifanya kama wewe ufanyavyo kwamba mpaka uwe na mengi ndipo ushukuru,basi ni dhahili ule muujiza using’elitokea. 
Maana ang’ekaa wee!! asubili apate samaki wengi na mijikate mingi,kisha ndipo ashukuru. Yakupasa kile ulichonacho sasa,ndicho umshukuru Mungu. Au kile unachokiona katika roho maana hicho ni chako,hicho hicho mshukuru Mungu.
▪ Nguvu hii,ndio ipatikanayo kwa yule mwenye kushukuru kwa moyo wake wote.
Kushukuru huleta nguvu ya ongezeko la kweli,pamoja na muujiza.
Bwana Yesu alipomshukuru Mungu katika ile mikate saba na visamaki,gafra pakawa na zidisho la mikate isiyokuwa na idadi pamoja na samaki walioweza kuwalisha wanaume elfu nne bila wanawake na watoto hata kubaki na masazo ya samaki na mikate katika makanda saba yamejaa.
Imeandikwa tena; ” Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia. 
Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma. ” Yoh.11:41-42
Bwana Yesu alipoenda kwa Lazaro aliyekuwa amekufa,tena yupo siku nne kaburini na ananuka. 
Hakumkemea shatani,wala hakuzivunja nguvu za shatani bali alitumia aina ya maombi ya kushukuru tu,ndiposa tunaona muujiza wa kufufuka kwa Lazaro unatokea. Kumbe kuna nguvu ya ajabu katika kushukuru.
Pata picha hii; Chukulia una watoto watatu wenye umri wa kufanana fana hivi,kisha ukagawa zawadi ya aina moja kwa kila mtoto. 
Kisha ukajiendea chumbani kwako upumzike,ile ujalala tu vizuri!unasikia mlango ukigongwa na kuangalia unamkuta mmoja wa watoto wako amerudi na kukushukuru kwa ile zawadi ambayo na wenzake wote walipata kama ile. Alafu wale wawili hakuja hata mmoja.
Nami ninakuambia,hakika utamuongezea huyu zawadi nyingine ikiwa ipo,au utajisikia bubujiko la kumfanyia kitu kingine kizuri zaidi tofauti na wenzake ambao hawana mpango wowote wa kushukuru. 
Na hivyo ndivyo mtu mmoja anapokuja kwa Bwana na kumshukuru kwa yote aliyotendewa,Mungu huongeza na kumfanyia miujiza mtu wa namna hiyo.
Usipitwe na Habari Yoyote Ya Injiri,Magazeti,mafundisho Ya Biblia,Mahusiano,Afya,Teknolojia Na Exclusive Interview on Togolay24 TV kila siku. Install Togolay24 App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

0 Maoni